2063
Miaka miwili iliyopita, nilifurahi kuona kuwa Umoja wa Afrika, wamechapisha hati ya Afrika tunayoitaka, yaani Ajenda 2063.
Kwa kipindi kirefu nimekuwa nikimwambia yeyote anayenisikiliza kwama moja ya vitu tulivyokosea wakati wa uhuru, ni kukosa mpango wa muda mrefu. Kwa mfano mpango wa miaka mia moja. Kwa upande mmoja, Ajenda 2063 inaonyesha kuwa pengine mimi sikuwa peke yangu kuwa na mtazamo huu.
Lakini ghafla nilijisikia vibaya nilipogundua kuwa hili chapisho lilifanyika mwaka 2014, na hivyo imenichukua miaka miwili kufahamu uwepo wake. Je, itachukuwa miaka mingapi kwa wahusika wote kulifahamu? Muda gani mpaka kupata matunda?
Sababu nyingine ya kujisikia vibaya, ni baada ya kusoma Ngũgĩ wa Thiong’o Decolonising the mind. Nyaraka zote zimeandikwa kwa kifaransa, kiarabu na kiingereza! Kwani zimukusudiwa watu gani? “Afrika tunayoitaka”, nani anasema? Viongozi, wanataaluma, wageni au sisi wote? Mbona sasa hazijachapichwa kwa lugha zetu?
Bila shaka, tunahitaji mawazo yaliyowekwa kwenye ajenda hii. Na ni muhimu pia kutambua kuwa mabadiliko yatakuja kwa hatua, lakini hatua zenye muelekeo sahihi ndizo zitakazo tufikisha kwenye lengo.