2019 kuelekea 2120: Rasimu ya ilani.
Ndiyo, kweli namaanisha mwaka 2120!
Nimeandika wazo dogo kuhusu ajenda ya Umoja wa Afrika. Lakini nikiangalia kwa umakini haya mawazo, hayanifurahishi. Nadhani tunahitaji sana mipango ya muda mrefu lakini miaka hamsini (50) haitoshi. Tunahitaji mpango endelevu, walau miaka mia moja kufikia lengo.
Hali ya sasa / Changamoto zetu
Ukiacha watu wachache wenye maslahi ya hali ya sasa, tuko wengi tunaotambua kuwa maisha yetu kama Waafrika yana changamoto nyingi.
Changamoto hizi zimekuwa nasi kwa miaka mingi. Na laiti tungetambua jinsi ya kukabiliana nazo mapema hali ya maisha yetu ingekuwa nzuri. Hata hivyo, hatujachelewa. Tunaweza kuzinduka kutoka kwenye usingizi wetu.
Changamoto za afya, elimu, ustawi na utaduni ni viamasishi vizuri vya maisha. Hivyo tuna motisha ya kupambana na magonjwa, ujinga na ufukara.
Afya zetu ni hafifu. Kuna sababu lukuki zinazosababisha hali hii. Uhaba wa watoa huduma, njia za kufikia huduma hizi, bima za afya, ufinyu wa uwekezaji na utafiti.
Elimu nyema ni chombo cha kutuwezesha kabiliana na changamoto hizi lakini hadi sasa elimu imebaki kuwa changamoto. Kwa mfano, ukosefu wa uhusihano wa maisha na masomo, lugha ya ufundishaji, vitabu na watoa elimu bila kusahau utamaduni wa kijumla.
Ustawi wetu umebaki kuwa ndoto isipokuwa kwa wachache kati yetu.
Utamaduni wetu una potea. Ni wazi kuwa utamaduni haupaswi kusimama bali mabadiliko ya jinsi jamii inavyo ishi yanahitaji kuhakisi matarajio ya jamii husika. Je, tunaweza kutunza jia zetu za maisha? Kutunza lugha, amali na thamani zetu? Kwanini jamii zetu zinachochea utengano?
Nini kifanyike?
Utambuzi wa uhalisi wa hali, ikiandamana na mtazamo sahihi, ni mwanzo mzuri. Hivyo, hatuhitaji kukata tamaa, bali tunahitaji ujasiri ili kufikia malengo yetu.
Tunahitaji mapinduzi. Bila mabadiliko ya kimsingi katika jinsi tunavyo tazama na kufikiria mambo hatuwezi kufanya chochote. Mabadiliko haya yanahitajika kuwa endelevu na ya kudumu kwa miaka mia kabla ya kuanza kufikiria kuwa tumepiga hatua.
Tunahitaji mapinduzi haya katika hatua tofauti: binafsi, kijamii na bara zima.
Katika hatua zote, tunahitaji kubadili mtazamo kutoka kutegemea kuokolewa na kutambua kuwa ni sisi wenyewe tunaweza kujiokoa. Na kama hatuamini tutazame historia yetu ya miaka 500 iliyopita. Hakuna mtu mwingine, kundi nje yetu au kitu chochote kinachoweza kutuokoa kama sisi wenyewe hatua chukua hatua. Tukiangalia historia, tunatambua kuwa, watu wanyonge wamekuwa wakishawishika kumngojea masiha atakaye badilisha maisha. Ila, mara zote huku kungojea hakukuleta mabadiliko.
Binafsi kama ilivyo kwa jamii, tuna wajibu wa kurekebisha mitazamo yetu ya mamlaka na utawala. Tofauti na jinsi Paulo angeweza kutuambia, nadhani, ni sahihi kutambua kuwa mamlaka yanatoka kwa watu, kutoka kwa kila mmoja wetu. Hivyo watawala wanahitaji kuwajibika kwa watu wao. Na wanajamii wana wajibu wa kuhakisha mamlaka tuliyowapa viongozi au vyombo vya uongozi yanatumika kujenga ustawi wetu.
Tunahitaji uchunguzi ili kutambua mambo yaletayo tija katika maisha yetu ya binafsi na maisha ya jamii yetu.
Hadithi ni muhimu sana. Hadithi ndio zinazoeleza maisha yetu, historia, mahusiano na vitu vingi. Tunahitaji hadithi mpya. Tunahitaji hadithi zinazoweza kutusaidia kupata nafasi yetu katika jamii. Hadithi zinazoweza kutupa moyo wa kuendelea kutafuta masuluhisho. Hadithi zenye kuchochea maelewano na maridhiano na kutuleta pamoja ili kushirikiana na kuishi pamoja. Tunahitaji hadithi zenye kumpa kila mmoja wetu sauti, na kutuwezesha kutoa mchango wake katika jamii na mwenendo wake.
Tunahitaji subira isiyo subiri. Tukianza sasa, tukiendelea na jitihada, basi katika miaka mia tutafikia malengo.